Madhara ya ugonjwa wa kisukari yanaepukika. Hatahivyo, ili kuepuka madhara ya kisukari kuna vitu unatakiwa uvifahamu.
Ingawa umeshindwa kujizuia kupata kisukari, unaweza kabisaa kuidhibiti sukari na kujikinga na madhara yake.
Ni muhimu unasoma makala hii kwasababu inaonesha unajali afya yako.
Nami nitakushauri ili kukuwezesha kufikia malengo yako. Kuwa na afya bora na kwa amani kama vile zamani-ingawa una kisukari.
Ili kueleweka vizuri, ninayagawa madhara ya kisukari katika makundi mawili nikilinganisha wakati gani yanaweza kutokea na kudumu.
Hivyo kuna makundi mawili ya madhara.
- Madhara yanayotokea ghafla, makali na ya muda mfupi. Sukari kushuka mwilini kuliko kawaida na sukari kupanda juu sana
- Madhara ya muda mrefu ya kisukari. Mfano kupata ganzi miguuni, kupungua kwa kuona na vidonda vya miguuni.
Endelea kusoma kufahamu madhara haya kwa undani na namna sukari inavyoyasababisha
Madhara Ya Muda Mfupi Ya Ugonjwa wa Kisukari
Sukari Ya Kushuka
Sukari ya kushuka (hypoglycemia) ni shida ya mara kwa mara kwa wagonjwa wa kisukari wanaotumia dawa aina ya sulfonylurea au insulini.
Sukari ya kushuka inaweza kusababisha upoteze fahamu au kukosa fahamu na inaweza kuhatarisha maisha.
Tunasema sukari imeshuka sana wakati ambapo mgonjwa hawezi kujitibu kwa kula au kunywa vyakula vya wanga ili kuongeza sukari kwenye damu.
Wagonjwa tofauti huwa na dalili tofauti wakati kiwango chao cha sukari kimeshuka. Hivyo kila mtu atatibiwa kulingana na dalili atakazo kuwa anazionesha.
Hatahivyo, kiwango cha sukari kwenye damu kikiwa chini ya 3.9 mmol/L (70 mg/dL), tunasema sukari imeshuka sana. Wakati huu mgonjwa atahitaji tiba hata kama hana dalilii.
Dalili za sukari ya kushuka
- maumivu ya kichwa njaa
- wasiwasi
- ganzi
- Kuhisi mapigo ya
- moyo
- kutokwa na jasho
- kutetemeka
- ugumu wa kuzungumza
- kuchanganyikiwa
- Kuyumba wakati wa kutembea
- Uchove mkali
- Kifafa
kukosa fahamu
Tiba ya sukari ya kushuka
Huduma ya kwanza kwa mtu amabye sukari yake imeshuka ni kula chakula cha wanga ikiwa mgonjwa anaweza kumeza.
Ikiwa mgonjwa anaweza kumeza chakula au kinywaji, anapaswa kula 15-20 g ya glucose.
Ikiwa glucose haipatikani, mpe kinywaji kilichotiwa sukari, vijiko 1-2 vya sukari, pipi 5-6 ngumu, au kikombe cha maziwa.
Ndani ya dakika 15 sukari itakuwa imeongezeka kwa 2.8mmol/L. Unaweza kurudia matibabu kama sukari bado itakuwa chini.
Ikiwa vyote hapo juu havipo, unaweza kumpatia vyakula vyovyote vyenye kabohaidreti (k.m. mkate, mchele, viazi).
Mpe mgonjwa chakula mara tu anapoweza kumeza chakula kwa usalama.
Kama mgonjwa kapoteza fahamu awahishwe hospitali kwa huduma ya ziada ya kitabibu.
Madhara ya kisukari: Sukari Kupanda Juu Sana
Sukari pia inaweza kupanda juu sana. Hali hii husababisha mgonjwa kupata hitilafu nyingi katika mfumo wa mwili na hivyo kuathiri mfumo wa ufahamu na kupumua.
Matibabu ya sukari kupanda sana yanafanyika katika kituo cha afya. Hatahivyo unaweza kutoa huduma ya kwanza.
Unapomuona mgonjwa wa kisukari mwenye dalili zifuatazo basi fahamu ya kwamba huwenda amepata madhara ya sukari kupanda sana kwa ghafla:
Dalili za sukari kupanda sana kwa ghafla
- Kusikia kichefuchefu, maumivu ya tumbo na kutapika
- Mgonjwa amekuwa mchovu ghafla na kupoteza fahamu au kutokujielewa. Wakati mwengine mgonjwa hubadilika badilika, kutokujielewa na kutopoteza fahamu.
- anahema kwa nguvu kwa kuvuta pumzi ndfu sana
- Kiwango cha sukari kinaweza kuwa 13.3mmol/L wakati mwengine hadi zaidi ya 33 mmol/L
Madhara Ya Muda Mrefu Ya Ugonjwa wa Kisukari
Sukari isipodhibitiwa kwa muda mrefu huaribu viungo mbalimbali muhimu na kusababisha kutokuhisi/ganzi, magonjwa ya figo, magonjwa ya moyo na ubongo kama kiharusi.
Madhara yote haya huweza kuendelea bila dalili mpaka yanapokuwa yamekuwa sugu. Hivyo ni muhimu sana kuhakikisha unafahamu hali yako ya afya kwa uhakika.
Madhara yote haya unaweza kuyadhibiti kama utachukua tahadhari katika muda muafaka.
Kabla ya kufahamu ufanye nini na upi ni wakati muafaka inabidi ufahamu kisukari husababishaje madhara haya.
Sukari inatakiwa ihifadhiwe kwenye tishu, isikae ndani ya damu. Inapokaa kwenye damu kwa kiwango kikubwa husababisha sumu inayofanya uharibifu kwa namna tatu.
1. Kwanza huaribu mishipa ya fahamu na hivyo hutoweza kuhisi. Kwa kuharibu mishipa ya fahamu husababisha sehemu zinazotegemea mishipa hii kutokufanya kazi kwa ufasaha.
Kwa mfano, upungufu / kosefu wa hisia miguuni husababisha mwenye kisukari kutokufahamu kama mguu umekandamizwa kama kubanwa na kiatu na hivyo kupelekea vidonda.
Vile vile kupungua ufanisi wa kazi za mishipa ya fahamu kwenye mishipa ya damu husababisha wangonjwa wa kisukari kupata matatizo ya presha kushuka na upungufu wa nguvu za kiume.
2. Kisukari pia huaribu mishipa ya damu na -kama tulivyoona- kusababisha hali inayoitwa artherosclerosis. Hatimaye mishipa ya damu huziba haswa ile ya pembeni ya mwili kama vile miguu.
Kukosekana kwa damu maana yake sehemu husika hukosa chakula, hewa safi na kinga.
Hivyo sehemu hiyo hufa na kama utapata maambukizi hutapona kwa urahisi. Mara nyingi hii imekuwa sababu kubwa ya wagonjwa wa kisukari kukatwa miguu.
3. Njia ya tatu, sukari huathiri kinga ya mwili kwa kuharibu na kupunguza muda wa kuishi wa seli zinazopambana na magonjwa.
Hali hii husababisha mgonjwa wa kisukari kuwa katika hatari ya kupata magonjwa hasa ya kuambukiza kwa urahisi na kushindwa kutibika kwa wakati.
- Muongozo kuhusu vyakula kudhibiti presha na kisukari. Bonyeza HAPA kusoma
Naepukaje Madhara Ya Muda Mrefu Ya Kisukari?
Ingawa kisukari husababisha vifo na ulemavu wa kudumu, kisukari hudhibitika pamoja na madhara yake kuepukika? Pata elimu sahihi
Moyo
Figo
Mishipa ya Fahamu
Vidonda Miguuni
Kinywa na meno
Moyo
Kadiri muda unavyokwenda kisukari kinaweza kuharibu mishipa yako ya damu na mishipa ya fahamu kwenye moyo. Fahamu kwa namna gani na vihatarishi vingine vya kupata ugonjwa wa moyo. Tafadhali, bonyeza HAPA
Figo
Kisukari huharibu figo kwa namna mbili: namna ya kwanza ni madhara ya moja kwa moja yatokanayo na uwepo wa kiwango kikubwa cha sukari kwenye damu. Fahamu namna ya kulinda figo lako. Bonyeza hapa
Mishipa ya Fahamu
Kisukari huathiri mishipa ya fahamu. Dalili hutegemea aina ya uharibifu na mshipa wa fahamu ni kama vile kusikia ganzi mikononi na miguuni, kushindwa kushiriki tendo la ndoa kwa jinsia zote nk. Linda mishipa yako ya fahamu. Bonyeza HAPA
Vidonda Miguuni
Vidonda miguuni vinawapata wengi wenye kisukari, na ni sababu inayoongoza kwa wagonjwa wa kisukari kukatwa miguu. Fahamu namna ya kutunza miguu yako. Bonyea HAPA
Kinywa na meno
Uwepo wa sukari nyingi huwapa uwezo wa Bakteria uwezo wa kukua na kustawi. Bakteria hawa husababisha meno kuoza na kutoboka. Na kama hujapata tiba haraka unaweza kupoteza jino kwa kung’oa. Fahamu namna ya kuwa na afya ya kinywa na meno. Bonyeza HAPA.
SAIDIA WENGINE
- Tutafurahi kusikia maswali au maoni yako kuhusu makala haya. Tafadhali tuandikie hapo chini.
- Tafadhali Like na Kusambaza Ujumbe Huu Kwa Watu Unaofikiri Watanufaika na Ujumbe Huu.